Hatimae beki wa pembeni kutoka nchini Ureno Nélson Cabral Semedo, ametua England na kujiunga na klabu ya Wolves, akitokea kwa manguli wa soka la Hispania FC Barcelona.
Semedo ameondoka FC Barcelona kufuatia kutokua sehemu ya mipango ya meneja mpya wa klabu hiyo Ronald Koeman, ambaye amedhamiria kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha Barca.
Beki huyo ametambulishwa rasmi kwenye kurasa za mitandao ya kijamii za Wolves na baadae alizungumza na waandishi wa habari, na huenda akaanza kuonekana kikosini mwishoni mwa juma hili, ambapo klabu hiyo itaendelea na mshike mshike wa Ligi Kuu ya England (EPL) dhidi ya West Ham Utd.
Meneja wa Wolves Nuno Espirito Santo, alikuwa sokoni akimtafuta mbadala wa Doherty ambaye amejiunga na Totenham siku chache zilizopita , hivyo kupatikana kwa Semedo anamini amefanikisha lengo lake.
“Mwaka jana walikuwa na msimu mzuri na ni timu nzuri hapa England na Ulaya kwa ujumla. Nina imani mwaka huu tutaweza kufanya mambo makubwa zaidi.”
“Nuno ni kocha mzuri. Amefanya mambo mazuri akiwa hapa Wolves na kwenye timu zingine. Nitajifunza zaidi kutoka kwake.” amesema Semedo wakati akifanya mahojiano na waandishi wa habari.
Kusajiliwa kwa beki huyo mwenye umri wa miaka 26, kimeigharimu Wolves kiasi cha pauni milioni 37 kama ada ya usajili, huku akisaini mkataba wa miaka mitatu,
Semedo anaondoka FC Barcelona, na kuacha kumbukumbu ya kuitumikia klabu hiyo katika michezo 124 na kufunga mabao 2.