Seneta wa chama cha upinzani nchini Bolivia, Jeanine Áñez amejitangaza kuwa Rais wa taifa hilo kufuatia hatua ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Rais, Evo Morales.
Anez amesema kuwa hatua ya kujitangaza kuwa Rais imezingatia matakwa ya Katiba ya nchi hiyo kwakuwa ndiye aliyekuwa wa pili kwenye matokeo ya uchaguzi. Mahakama ya Kikatiba ya Bolivia imebariki hatua hiyo; na Anez ameahidi kuitisha uchaguzi wa kidemokrasia hivi karibuni.
Hata hivyo, amepata upinzani mkali kwa hatua aliyoichukua. Wabunge kutoka katika chama cha Morales walisusia bunge na rais huyo wa zamani alitangaza alichokifanya Anez kama mapinduzi ya Serikali.
Morales amekimbilia nchini Mexico ambako amedai aliomba hifadhi kwakuwa maisha yake yalikuwa hatarini.
Rais huyo wa zamani alijiuzulu nafasi ya Urais Jumapili iliyopita ikiwa ni wiki kadhaa tangu yazuke maandamano makubwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu. Alisema kuwa aliamua kujiuzulu mwenyewe ili kuepusha damu kumwagika.
Jana, upande wa Anez ulidhibiti bunge na kumpitisha kuchukua nafasi ya urais kwa kipindi cha mpito. Hatua hiyo ilipingwa vikali na wabunge wanaomuunga mkono Morales ambao hadi leo wamekuwa wakipinga.