Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kutoa ushirikiano, ili kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika Agosti 28 mwaka 2022.
Amesema takwimu zitakazopatikana katika zoezi hilo zitatumiwa na Serikali katika utungaji, ufuatiliaji na uboreshaji wa sera mbalimbali pamoja na kufanya maamuzi kwa kuzingatia vigezo vya kitakwimu.
Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa kitabu cha mkakati wa usimamizi na utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Aidha, amesema takwimu rasmi zitaiwezesha Serikali kukabiliana na changamoto mbalimbali zitakazojitokeza katika sekta zote za kiuchumi, kwa kuwa zitatoa viashiria vya uwajibikaji ndani ya Serikali.
Waziri Mkuu Majaliwa amezielekeza taasisi zote za Serikali kutoa ushirikiano unaohitajika kwa lengo la kufanikisha zoezi hilo kwa haraka.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amesema kuwa, hana shaka na utendaji kazi wa ofisi za takwimu za Tanzania Bara na Zanzibar, kwani ushirikiano wao ulifanya sensa ya mwaka 2012 kuwa bora Barani Afrika.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wa kutosha, kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa mafanikio.