Mkuu wa mkoa Morogoro, Fatma Mwasa akiwa ni miongoni mwa Wananchi waliohesabiwa kwenye zoezi la sensa hii leo Agosti 23, 2022 ametoa wito kwa wanaume kuacha kuficha taarifa za wake zao hatakama wana zaidi ya mmoja, ili kusaidia kuondoa migogoro wakati ufatiliaji wa mirathi.
Mwasa ameyasema hayo mara baada ya kukamilisha zoezi la kuhesabiwa, ambapo amesema familia nyingi zimekua na migogoro kutokana na baadhi ya wanaume kuwaficha wake zao taarifa muhimu ikiwemo kuwa na mke au mtoto nje ya familia anayoishi nayo na kuleta sintofahamu msibani.
“Kuna ndoa zile zinazofahamika kisheria yaani za kiserikali au za kidini sasa kuna wale wengine ambao wanaishi na familia mbazo bado hazijatambulika kisheria niwaombe wawe wakweli kwa makarani hii itasaidia kuondoa sintofahamu wakati wa misiba na kuepusha mambo yanayoweza kuzuilika,” amesema Mwasa.
Aidha, amewataka Wananchi kuwa wakweli katika utoaji wa taarifa zao kwa Makarani, ili kuweza kusaidia kufahamu viwango vya maisha kwa kila Mtanzania na kujua ni aina gani ya uchumi tulionao.
“Ukiulizwa una kazi gani kama huna kazi basi we sema sina ila ukisema una kazi Serikali inajua kuna unafuu wa ajira wakati huna hivyo ifike mahali kila mtu acheze eneo lake kwa uaminifu ili kufikia lengo kusudiwa,” amebainisha Mkuu huyo wa Mkoa.
Hata hivyo amewataka wananchi kutambua zoezi hilo ni muhimu na limetumia gharama kubwa kuliandaa hivyo kwa wale ambao sio waaminifu waache matukio ya uharibifu kwa kuepuka wizi wa aina mbalimbali kikiwemo vishkwambi vya Makarani wa Sensa.
Amesema, “Sheria ipo na yeyote atakayekwenda tofauti au kuvuruga zoezi hili vyombo vya usalama vipo atakamatwa na kufikishwa Mahakamani maana zoezi hili limeigharimu Serikali pesa nyingi sana katika uaandaji sasa wale ambao sio waaminifu waache mara moja la sivyo watashughulikiwa,”
Mkuu huyo pia amewapongeza Makarani kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo kutuinza siri na taarifa za Watu kama walivyokula kiapo kabla ya kazi na kuwaomba wananchi kuwa na subira hadi watakapo wafikia na kuwapa ushirikiano ili kukamilisha zoezi hilo la kitaifa la Sensa na makazi ya watu.