Wafanyakazi wametajwa kuwa na uhakika wa kinga na kipato kutokana na majanga yanayosababishwa na ajali, magonjwa na vifo kazini, kufuatia uwepo wa Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi (WCF) ambao ni hatua muafaka katika mazingira ya sasa.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma hii leo Septemba 26, 2022 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule wakati akifungua mafunzo ya tathmini za ulemavu uliosababishwa na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kwa madaktari wa mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma.
Amesema, “Katika hali ya kawaida ongezeko litakwenda sambamba na ongezeko la matukio na athari zinazotokana na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi hivyo jukumu la WCF sio kulipa Fidia pekee bali pia kushirikiana na wadau katika kubuni na kuendeleza mbinu za kupunguza au kuzuia ajali na magonjwa yatokanayo na kazi.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema wanajivunia kufanya vizuri katika uboreshaji wa mifumo ya kielektroniki ya utoaji huduma pamoja na punguzo la kiwango cha uchangiaji kwa sekta binafsi kutoka asilimia 0.6% hadi 0.5% na punguzo kubwa la riba kwa madeni ya michango ya nyuma.
Amesema, Maboresho hayo yanalenga kukuza uzalishaji ambapo sasa Waajiri wa Sekta binafsiwamepewa nafuu kubwa ya kuelekeza nguvu katika uzalishaji mali, huku WCF ikiendelea kulinda nguvukazi ya Taifa.
Mafunzo hayo, yameandaliwa na WCF kama sehemu ya hatua muhimu kuuwezesha kutekeleza vyema jukumu la kufanya tathmini sahihi na hatimaye Fidia stahiki pindi mfanyakazi anapoumia au kuugua kutokana na kazi.