Afisa Mtendaji Mkuu wa Young Africans amejitosa kwenye sakata la kampuni ya GSM kudhamini zaidi ya klabu moja zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Kampuni ya GSM imekua ikijadiliwa sana katika mitandao ya kijamii na wengine wamefikia hatua ya kuituhumu kuharibu soka la Tanzania, kwa kushawishi timu zicheze kwa kukamia hasa zinapoklutana na Mabingwa watetezi Simba SC.
Senzo amesema kinachoendelea kwenye mtandao kuhusu kampuni ya GSM kinapaswa kukemewa haraka na ikiwezekana kilaaniwe, kwani kinaharibu taswira ya mchezo wa soka nchini Tanzania.
Senzo amesema: “Ni kwa masikitiko makubwa kwamba tunasoma mijadala inayomshambulia mfadhili na mdhamini wetu bila sababu za msingi”
“Mtazamo ambao unaoneshwa na wafanyakazi wa vyombo vya Habari (Wachambuzi) na watu binafsi Kuelekea kwa watu wenye sifa nzuri wanaoleta pesa kwenye soka ULAANIWE”
“Haiwezekani kuwa katika nyakati hizi za majaribu ambapo wafadhili hawajitoi sana kudhamini soka, kuna watu binafsi wanawashambulia watu walewale ambao wanatumia pesa zao kusaidia soka”
“Je ni kwa sababu Yanga imeimarika na kufanya vizuri chini ya ufadhili wa (GSM) ndio maana baadhi ya watu wanaona kuna haja ya kumshambulia mfadhili wetu ?”
“NATAHADHARISHA, Ujinga huu usiachwe uendelee, nashauri kwamba ushughulikiwe mara moja na vyombo vinavyohusika”
“Kuna ubaya gani (GSM) kuvisaidia vilabu vingine vinavyohitaji usaidizi ?”
Hoja wanazotoa ni dhaifu sana, zenye lengo la kuleta usumbufu na hofu kwa (GSM)”
“Kilichokuwa kinaendelea ni dalili kuwa brand ya (GSM) inakuwa na inasumbua wengine huko sokoni”
“Naomba watu waiunge mkono (GSM) kwa uwekezaji kwenye soka ambayo ni moja ya nguzo muhimu za kijamii katika ustawi wa Tanzania”
Mbali na kuidhamini na kuifadhili Young Africans Kampuni ya GSM inafanya hivyo kwenye klabu za Coastal Union na Namungio FC ambazo zinashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Tayari klabu hizo zimeshakutana na Simba SC na zilionesha kupambana ndani ya dakika 90, halia mbayo imechangia kuibua mijadala ya kuihusisha GSM kushawishi mabingwa watetezi kukamiwa ili wapoteze mchezo.