Uongozi wa klabu ya Young Africans umeanza maandalizi ya kuelekea mchezo wa mkondo wa pili, wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United, utakaopigwa mwishoni mwa juma hili nchini Nigeria.
Young Africans walipoteza mchezo wa mkondo wa kwanza jana Jumapili (Septemba 12), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kwa kufungwa bao 1-0.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa, Afisa Mtendaji Mkuu Senzo Mazingiza anajiandaa na safari ya kuelekea Nigeria kwa ajili ya kuweka mambo sawa, ili kuepuka changamoto ambazo huenda zikawakwamisha wakati kikosi chao kitakapowasili nchini humo.
Inadaiwa kuwa Senzo ataambatana na mpishi maalum wa Young Africans atakaekuwa na jukumu la kuawaandaliwa chakula wachezaji na baadhi ya viongozi watakaoambatana na timu hadi Nigeria, kwa ajili ya mchezo wa mkondo wa pili.
Kikosi cha Young Africans kinatarajiwa kuanza safari ya kuelekea Nigeria juma hili, tayari kwa mchezo wa mkondo wa pili ambao utachezwa Jumapili (Septemba 19), Uwanja wa Yakubu Gowon, mjini Port Harcourt katika jimbo la Rivers.