Afisa Mtendaji Mkuu wa Young Africans Senzo Mazingiza Mbatha, amesema Uongozi wa klabu hiyo hauna mshawasha na mchezo dhidi ya Simba SC utakaochezwa kesho Jumamosi (Desemba 11), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo ambao umepangwa kuanza saa Kumi na Moja Jioni, huku Mwamuzi Herry Sasii akitajwa kuwa msimamizi wa sheria 17 za soka.
Senzo amesema wanatambua kuhusu mchezo huo kwa kuwa upo kwenye ratiba, hivyo watafanya maandalizi mazuri ili kupata ushindi.
“Ipo wazi kwa muda mrefu kwamba lazima tutakutana na Simba SC kwenye mchezo wa ligi hivyo hakuna Presha kuelekea mchezo huo, kila kitu kinakwenda sawa na maandalizi yake ni kama ilivyo kwenye michezo mingine.”
“Mwendo ambao tunakwenda nao nina amini kwamba mashabiki wanaona hivyo hakuna haja ya kuwa na mashaka juu ya uwezo wa wachezaji wetu, kwani kila mmoja anafanya kazi kwa umakini katika kutimiza majukumu yake,” amesema Senzo
Young Africans inaongoza Msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 19, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 17, baada ya kila timu kucheza michezo saba.