Mshauri wa Masuala ya Mabadiliko ndani ya Klabu ya Young Africans Senzo Mazingiza Mbata amesema mchezo wa Jumamosi (Mei 08) utatawaliwa na visasi kutokana na matokeo ya michezo iliyopita.

Senzo ambaye alikua Afisa Mtendaji Mkuu Simba SC msimu uliopita kabla ya kuhamia Young Africans mwaka 2020, amesema licha mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini Tanzania kutarajiwa kuwa na visasi pia utakuwa mgumu.

Amesema kupoteza kwa Simba SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Young Africans ni sehemu ya kisasi ambacho anakitazama kama chagizo la ushindani anaoutarajiwa ndani ya dakika 90, ambazo zitaamua nani ataondoka na alama tatu muhimu siku hiyo ya Jumamosi (Mei 08).  

“Tuliwafunga kwenye Kombe la Mapinduzi, tukaja tukatoka nao sare kwenye mchezo wa raundi ya kwanza, lakini mechi mbili za msimu uliopita walishindwa kupata matokeo ni wazi naona kabisa safari hii watahitaji kulipa kisasi na ndipo ugumu utakapokuwepo,”

“Ugumu mwingine wa mchezo huu ni kwamba ukiangalia tupo kwenye mbio za ubingwa na tunafukuzana kwenye msimamo, wenzetu wakiongoza na sisi tukifuata kwa tofauti ndogo tu,”

“Morali kwa upande wetu imeongezeka baada ya kupata ushindi katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons, awali tulikuwa hatupo vizuri sana lakini morali imerejea kwa wachezaji.” Amesema Senzo Mazingiza

Simba SC inaongoza msimamowa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 61, ikifuatiwa na Young Africans yenye alama 57 huku Azam FC wakishika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 54.

Morrison apigiwa chepuo la kuikabili Young Africans
Watu 87 wanusurika kifo baada ya meli kukwama mchangani