Mshauri wa Young Africans katika Mfumo wa Mabadiliko ndani ya klabu hiyo Senzo Mazingiza Mbatha, amewataka viongozi wenzake kusitisha furaha ya kuifunga Simba SC, na kufikiria namna ya kushinda michezo ya Ligi iliyosalia.
Senzo ameomba suala hilo, baada ya kuona furaha iliyozidi kikomo kuendelea kushamiri miongoni mwa viongozi, mashabiki na wanachama tangu walipomalizana na Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu Jumamosi (Julai 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Kiongozi huyo raia wa Afrika Kusini amesema ipo haja ya kujipanga kuelekea michezo yao miwili iliyosalia upande wa Ligi Kuu kwa msimu huu, kabla ya kukutana tena na Simba SC mjini Kigoma katika mchezo wa Fainali wa Kombe la Shirikisho (ASFC).
“Furaha inatakiwa ifike tamati na mambo mengine yaendelee, tunatakiwa kushinda michezo miwili ya Ligi ilizobaki.”
Kuhusu mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho (ASFC), Senzo amesema utakua mchezo mgumu na hatarajii mambo yatakuwa kama ilivyokua Julai 03.
Amesema Simba SC watahitaji kushinda mchezo huo ili kuwapoza machungu Mashabiki na Wanachama wao, hivyo Uongozi wa Young Africans hauna budi kujipanga kwa mapambano.
“Simba hawatakuja kirahisi katika mchezo ujao utakuwa mgumu mara tatu wa huu uliopita, hutakiwi kuingia katika mchezo huo na kumbukumbu za kushinda mchezo uliopita, tunatakiwa kufuta na kusahau kama tulishinda.”
Young Africans ilitinga fainali ya ASFC kwa kuifunga Biashara United Mara FC bao 1-0 mjini Tabora, huku Simba SC wakiitandika Azam FC bao 1-0 mjini Songea.