Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ametaka Sheria, Mifumo na Sera zinazohusiana na mabadiliko ya Kiteknolojia ilete matokeo chanya yatakayomsaidia Kijana Mbunifu wa Kitanzania kuweza kupiga hatua maishani.
Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya AZAKI jijini Dar es Salaam na kudai kuwa Vijana wengi waliojaribu kusonga mbele kupitia ubunifu wao, wameshindwa kufanikiwa kutokana na mifumo iliyopo, huku wale wanaojitahidi kupambana na hali halisi wakikatishwa tamaa.
“Utakuta kijana amepambana kabuni kitu au kaanzisha kitu, lakini sasa mifumo inamuangusha sheria zinambana, kuna kodi kuna leseni kuna vitu vingi na hapati usaidizi au kuoneshwa njia apite wapi, ipo haja ya watunga sera wetu na wasimamizi wa sheria kuhakikisha wanalitazama hili,” amesema Dkt. Ndugulile.
Hata hivyo, Ndugulile pia ameongeza kuwa Mamlaka zenye udhibiti zinatumika vibaya na si rafiki kwa kufanikisha mambo kwani zinatakiwa kulea badala ya kuzuia kwani wakati uliopo unawahitaji wabunifu wenye kulisaidia Taifa na ni lazima kuendana na wakati.