Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amewataka wadau wa elimu nchini kuipitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kutoa maoni yatakayowezesha serikali kuandaa au kuboresha Sera hiyo ambayo inakwenda sambamba na uboreshaji wa mitaala ya elimu.

Waziri Mkenda ameyasema hayo leo Machi 30,2022 jijini Dodoma wakati  wa mkutano wa kupokea maoni kuhusu uboreshaji wa mitaala na sera ya elimu kutoka kwa viongozi wa Dini pamoja na wamiliki wa shule binafsi.

Aidha Waziri Mkenda amesema kuwa ameunda kamati ya wataalamu ili wakafanyie mapitio sera hiyo ili kujua ni kwanini sera haitekelezwi tangu ilipopitishwa mwaka 2014 ambayo inamajibu mengi ya maswali yanayoendelea kuibuka kuhusu ubora wa elimu yetu.

Amesema kuwa lengo la serikali ni kuwa na sera itakayoakisi mahitaji halisi ya ubora wa elimu na amebainisha kuwa mwezi wa tano mwaka huu 2022 wanatarajia kupokea rasimu ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau wa elimu namna ya kuboresha elimu hapa nchini.

“Ukiangalia mapendekezo ya wadau wengi ni wanataka elimu ya lazima iwe miaka 10 na Sera yetu ya mwaka 2014 inataka mwanafunzi mara baada ya kupata elimu ya awali inatakiwa apate elimu ya lazima kwa miaka 10 ili kumuwezesha mwanafunzi kujua kusoma, kuandika kuhesabu na kupata maarifa ujuzi ya elimu ya ufundi stadi,” Amesema Waziri Mkenda.a

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Prof. Carolyne Nombo amewashukuru Viongozi wa Dini na Wamiliki wa Shule binafsi kwa kushiriki katika mkutano huo muhimu wa kutoa maoni ambayo yatasaidia kuboresha Sera na Mitaala ili watoto wa Kitanzania wapate elimu itakayowapatia ujuzi na kwa kuzingatia maadili ya Kitanzania.

Naye  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dkt.Aneth Komba amesema kuwa maboresho ya mitaala unashirikisha makundi yote na katika kuboresha sera ya elimu na mitaa wanajifunza pia kupitia nchi zilizofanikiwa zaidi kuona namna wanavyoendesha elimu yao.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Dini na wamiliki wa shule wamesema elimu ni msingi wa kila kitu hivyo pamoja na mambo mengine umakini kwenye lugha ya kufundishia unahitajika kwa kuhakikisha lugha ya Kiswahili na Kingereza zinatumika

Urusi na Ujerumani wajadili malipo ya gesi kwa Rubles
Bluce Willis kutoonekana tena kwenye filamu