Mwanadada kutoka nchini Marekani, Serena Williams ameendelea kupeta katika michuano ya Tennis, ya Wimbledon Open kwa kujikatia tiketi ya kucheza hatua ya nusu fainali.

Serena, amesonga mbele kwenye michuano hiyo inayoendelea jijini London nchini England, kufuatia ushindi wa seti mbili kwa moja aliouvuna kutoka kwa mpinzani wake Victoria Azarenka ambaye ni raia wa nchini Belarus.
Serena alimshinda Azarenka kwa 3-6, 6-2 na 6-3.

Ushindi huo unamuwezesha Serena kufanya maandalizi ya kutosha kufuatia mlima mrefu wa kupanda unaomuandama katika hatua ya nusu fainali ambapo atapambana na mpinzani wake wa karibu, Maria Sharapova ambaye ni raia wa nchini Urusi.
Sharapova alipata tiketi ya kutinga kwenye hatua ya nusu fainali baada ya kumshinda Colleen “CoCo” Vandeweghe, kutoka nchini Marekani.

Ushindi wa seti mbili kwa sifuri ambazo ni 7-6 na 7-6 ndio ulikuwa chagizo kwa Sharapova la kwenda kupambana na Serena katika mchezo wa hatua ya nusu fainali.

Kwa upande wa wanaume michuano hiyo itaendelea katika michezo ya hatua ya robo fainali hii leo ambapo:
. Vasek Pospisil kutoka nchini Canada atapambana na Andy Murray kutoka nchini Scotland.
. Novak Djokovic kutoka nchini Serbia atapambana na Marin Čilić kutoka nchini Croatia
. Gilles Simon kutoka nchini Ufaransa atapambana na Roger Federer kutoka nchini Uswiz.
. Stan Wawrinka kutoka nchini Uswiz atapambana na Richard Gasquet kutoka nchini Ufaransa

Mo Farah Kurejea Dimbani Baada Ya Kashfa Nzito
Chelsea Yazipiga Kanzu Klabu Nguli Barani Ulaya