Timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) itaondoka mjini Rabat-Morocco kesho kuelekea Cameroon kuendelea na kambi ya siku nane.
Serengeti Boys wataondoka Morocco baada ya kuweka kambi kwa zaidi ya majuma matatu, huku wakicheza mchezo miwili ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya wenyeji wa fainali za Afrika kwa vijana Gabon.
Katika michezo hiyo, Serengeti Boys walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja, hali ambayo imeendelea kuonyesha mlolongo mzuri wa maandalizi ya fainali za Afrika zitakazoanza Mei 14.
Katibu mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF, Celestine Mwesigwa amezungumza na Dar24 na kueleza mipango ya safari kwa timu hiyo kutoka Morocco kuelekea Cameroon.
Mwesigwa amesema mipango ya safari ipo vizuri na TFF inaamini michezo mingine miwili ya kirafiki dhidi ya Cameroon, itaendelea kuimarisha umakini wa Serengeti Boys kabla ya kutua nchini Gabon kuanza kampeni ya kusaka ubingwa wa Afrika pamoja na nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia kwa vijana.
“Tunaamini michezo dhidi ya Cameroon itaendelea kuwaimarisha vijana wetu, tumefanikiwa kutimiza matakwa ya benchi la ufundi kwa kufanikisha michezo kadhaa ya kirafiki kabla ya kuelekea kwenye mashindano, tunaamini hali hii itawasaidia vijana kufanya vizuri watakapokua Gabon.” Amesema Mwesigwa.
Kabla ya kuelekea Rabat-Morocco Serengeti Boys ilicheza michezo ya kirafiki dhidi ya Burundi mara mbili ambapo katika mchezo wa kwanza walishinda mabao mawili kwa sifuri.
Mchezo wa pili walishinda mabao matatu kwa sifuri. Kisha walicheza dhidi ya Ghana na kulazimisha matokeo ya sare ya mabao mawili kwa mawili.
Katika fainali za Afrika kwa vijana, Serengeti Boys imepangwa kundi B sambamba na Ethiopia, Niger na Angola.
Kundi A lina timu za Gabon, Ghana, Cameroon na Guinea.