Kutoka kwa Masau Bwire.
Timu yetu ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, leo Alhamis, August 16, 2018 wanatupa karata yao ya pili dhidi ya Sudani katika mashindano ya kufuzu Afcon kwa vijana U17, Kanda ya CECAFA (CECAFA U17 Afcon Zonal qualifier ).
Katika mchezo wa awali, Serengeti boys ilipata ushindi wa magoli 2-1 dhidi ya Burundi.
Timu yetu ya Serengeti boys katika mchezo wa leo, inahitaji matokeo chanya, ya point 3 ili iweze kuongoza kundi na hatimaye iweze kusonga mbele, hatua inayofuata hadi kuwa mabingwa wa mashindano hayo.
Vijana hawa hakuna asiyejua kuwa ni wazuri, wataalam na wajuzi wa kucheza mpira, wanajua sana, wanachokihitaji ni kushangiliwa tu wanapocheza ili waoneshe umahiri wao katika kusakata Kandanda.
Watanzania wenzangu, wadau, wapenzi na mashabiki wa soka, ebu tuwaunge mkono vijana wetu, tujitokeze leo kwa wingi uwanja wa Taifa, Dar Es salaam, Saa 10.00 jioni, tukawashangilie vijana wetu ili tuwezeshe ushindi katika mchezo wa leo.
Itakuwa aibu, tena aibu si tu ya mwaka, ya milele, katika mchezo wa leo muhimu, Sudan, wageni wawe na washangiliaji wengi katika uwanja wetu wa nyumbani kuliko sisi.
TFF kwa kutambua umuhimu wa mashindano hayo, wamepambana kweli, kweli kuhakikisha mashindano hayo, watazamaji wanaingia bure, lengo likiwa Watanzania tuingie kwa wingi uwanjani kuwashangilia vijana wetu.
Niwasihi na kuwaomba sana Watanzania wenzangu, niwaombe tena na tena, tujitokeze leo kwa wingi mno, twende uwanja wa Taifa, tukawashangilie vijana wetu kuhakikisha ushindi unapatikana.
Mashindano kama hayo, Kanda ya Africa yatafanyika mwakani, bingwa wa mashindano haya yanayoendelea ndiye itaiwakilisha Kanda ya CECAFA katika fainali za mashindano ya Afcon U17 Kanda ya Africa, ambayo mpaka sasa mwandaaji ni Tanzania.
Mwandaaji hupata fursa ya kushiriki moja kwa moja katika mashindano anayoyaandaa, sisi Watanzania mpaka sasa fursa hiyo tunayo lakini hztupaswi kuitegemea kwa asilimia zote, kwani tukinyang’anywa uandaaji, hatutashiriki endapo tutakosa ubingwa katika mashindano haya yanayoendelea.
Tunahitaji ubingwa katika mashindano haya, ili tuwe na uhakika wa asilimia zote kushiriki mashindano ya U17 Africa.
Shime Watanzania, chonde, chonde, ebu twende uwanjani leo, ni bure tu, hakuna kiingilio, tukawashangilie vijana wetu, ushindi dhidi ya Sudani upatikane, tena wa kishindo.
Mungu ibariki Tanzania….
Mungu ibariki Serengeti boys….
Masau Kuliga Bwire – Mzalendo.