Kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) imeanza maandalizi ya kujiwinda na michuano ya vijana ya kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA U17) inayotarajiwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu nchini Botswana.
Taarifa iliyotolewa na shirikisho la soka nchini TFF kupitia idara ya habari na mawasilino imeeleza kuwa, kikosi cha Serengeti Boys kiliingia kambini mwishoni mwa juma lililopita katika hosteli za shirikisho hilo, Uwanja wa Karume uliopo Ilala mjini Dar es Salaam.
Mkuu wa idara ya habari na mawasilino ya TFF Clifford Mario Ndimbo amesema kikosi kipo chini ya Kocha Mkuu, Oscar Milambo anayesaidiwa Maalim Saleh ‘Romario’ na kocha wa makipa, Manyika Peter.
Ndimbo amesema michuano COSAFA U17 ambayo Serengeti Boys itashiriki kama mgeni mualika itakua sehemu ya maandalizi ya fainali za Afrika za chini ya miaka 17 zitakazofanyika nchini Tanzania mwaka 2019.