Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Wasichana chini ya Umri wa miaka 17 ‘Serengeti Girls’ Bakari Shime amesema kikosi chake kipo tayari kuikabili Canada kwenye mchezo wa mwisho hatua ya Makundi leo Jumanne (Oktoba 18), katika Fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini India.

Serengeti Girls ina kazi ya kuhakikisha inashinda mchezo huo, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza hatua ya Robo Fainali, huku ikishinda mchezo uliopita dhidi ya Ufaransa mabao 2-1.

Kocha Shime amesema kikosi chake kimekamilisha maandalizi ya kuelekea mchezo huo utakaoanza saa kumi na moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki, huku akimini kupata matokeo yatakayowavusha.

Amesema katika maandalizi ya kuelekea mchezo huo amejitahidi kufanya maboresho kwenye kikosi chake kwa kupunguza kama si kumaliza changamoto alizoziona kwenye mchezo uliopita dhidi Ufaransa.

“Kuna mapungufu truliyaona kama Benchi la Ufundi kwenye mchezo wetu uliopita, tumejaribu kuyafanyia kazi ili kuwa bora zaidi kwenye mchezo ujao, ambao tunajua utakua mgumu zaidi.”

“Malengo yetu ni kufanya vizuri kadri ambavyo itawezekana, wito wangu kwa watanzania ni kutuombea, naamini tunaweza kuvuka hatua ya makundi,” amesema Kocha Shime

Endapo Serengeti Girls itashinda dhidi ya Canada, itafikisha alama sita ambazo zitawawezesha kutinga hatua ya Robo Fainali nyuma ya Japan iliyojizoela alama sita baada ya kucheza na kushinda michezo miwili dhidi ya Tanzania na Canada.

Wakati Tanzania na Canada zikicheza, Ufaransa na Japan nazo zitakua zikiumana muda huo huo ili kuepusha dhana ya upangaji wa matokeo.

Mwinyi Zahera: Ibrahim Ajibu bado wamo
Hatma ya Urais wa Uganda ipo mikononi mwa Wananchi: Museveni