Kikosi cha Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Umri wa miaka 17 ‘Serengeti Girls’ kinaendelea na maandalizi ya Fainali za Kombe la Dunia 2022, zitakazofanyika baadae mwaka huu nchini India.
Serengeti Gilrs itashiriki Fainali hizo kwa mara ya kwanza, baada ya kufuzu ikitokea Barani Afrika ambako ilizifunga timu za taifa za Cameroon, Botswana na Burundi.
Kocha Mkuu wa timu hiyo Bakari Shime amesema kikosi chake kinaendelea vizuri na maandalizi huko visiwani Zanzibar, hukua kiwa na matumaini makubwa ya kwenda kufanya vizuri.
Amesema wachezaji aliowaita kikosini wanaonyesha kujituma na kufuata maelekezo yake, hivyo amewatoa hofu Mashabiki wa Tanzania kwa kuwaambia wawe na imani timu yao.
“Tumeanza kujiandaa mapema na Fainali za Kombe la Dunia ili kupata muda mzuri wa kuwa na kikosi imara na bora kuelekea kwenye michuano hii, ambayo ninakiri ina changamoto kubwa ya ushindani,”
“Maendeleo ya Wachezaji wangu ni makubwa sana, wanajituma na kufuata maelekezo yangu ninayowapa, nina imani tunakwenda kupambana na kufanya vizuri katika Fainali za Kombe la Dunia kule India.”
“Watanzania wanapaswa kuendelea kuwa imani na timu yao, waendelee kuiombea, niwahakikishie hatutawaangusha kwa sababu hadi sasa nafasi ya kutwaa ubingwa ipo wazi kwa timu yoyote shiriki.” amesema Bakari Shime
Serengeti Girls imepangwa Kundi D Sambamba na nchi za Japan, Canada na Ufaransa.
Timu hiyo itaanza kusaka ubingwa wa Dunia kwa kucheza na Japan Oktoba 12 , kisha itacheza dhidi ya Ufaransa Oktoba 15 na kumaliza hatua ya Makundi kwa kupapatuana na Canada mnamo Oktoba 18.
Michezo ya Kundi D imepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Pandit Jawaharlal Nehru, uliopo mjini Margao.