Mshambuliaji wa kutumainiwa wa klabu ya Man City, Sergio Aguero huenda akakaa nje ya uwanja kwa muda wa mwezi mmoja, kufuatia jereha la misuli ya paja alilolipata akiwa na kikosi cha timu ya taifa lake la Argentina.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alipatwa na mkasa wa maumivu wa misuli ya paja alipokua kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, dhidi ya timu ya taifa ya Ecuador.

Aguero, alihojiwa na kituo cha TyC Sports mjini Buenos Aires nchini Argentina alipo sasa kwa mapumziko na alisisitiza huenda akawa nje kwa muda wa mwezi mmoja kutokana na maelezo aliyoyapata kutoka kwa madaktari walimfanyiwa vipimo.

Kuumia kwa mshambuliaji huyo ambaye alifunga mabao matano wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England dhidi ya Newcastle Utd, huenda kukawa pigo kubwa kwa Man City katika kipindi hiki ambacho kinashuhudia klabu hiyo inapambana kwenye mashindano zaidi ya ligi kuu.

Aguero, atakosa michezo minne ya ligi ya nchini England, pamoja na michezo miwili ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya  Sevilla.

Kuwa kwake nje, kunamfanya meneja wa klabu ya Man City, Manuel Pellegrini kuwa na matumaini ya kumtumia mshambuliaji kutoka nchini Ivory Coast, Wilfried Bony kama mshambuliaji wa kati huku akimtegemea kinda Kelechi Iheanacho kama mbadala wake.

Phil Jagielka Kuvaa Kitambaa Cha England
Magufuli Aunda Timu Mpya Ya Kazi