Nahodha na Kiungo wa FC Barcelona Sergio Busquets amesema atamrudishia kitambaa cha unahodha Mshambuliaji Lionel Messi, endapo atafanikiwa kurejea klabuni hapo msimu ujao wa Ligi Kuu ya Hispania ‘

La Liga.

Messi ambaye kwa sasa anaitumikia PSG ya Ufaransa, anahusishwa na mpango wa kutaka kurudi FC Barcelona, kufuatia mambo kumuendea kombo tangu alipotua jijini Paris-Ufaransa mwanzoni mwa msimu huu.

Tetesi za Messi kurejea FC Barcelona ziliibuka, kufutia klabu ya PSG kuwa mbioni kumpoteza Kylian Mbappe anayetarajiwa kwenda Real Madrid, jambo ambalo linaonyesha kumkera Mshambuliaji huyo ambaye alivutiwa kucheza na kinda hilo la Ufaransa.

Kuibuka kwa tetesi hizo, kulimfanya meneja wa FC Barcelona Xavi kutangaza kufungua milango kwa Lionel Messi kurejea Camp Nou, ili kurudisha hali yake ya furaha ambayo kwa sasa inaendelea kupotea.

Hatua hiyo iliungwa mkono na Nahodha wa sasa wa FC Barcelona Sergio Busquets alipoelezea hamu yake ya kutaka kuona wakicheza sambamba na mshindi huyo mara saba wa Tuzo ya Ballon d’Or.

“Bila shaka namkumbuka. Ndani ya uwanja na nje ya uwanja,” Busquets alisema kuhusu Messi katika mahojiano na kituo cha redio cha Hispania, RAC1.

“Hakuna mtu mwingine ambaye ametupa kile alichotupa. Alifanya mabadiliko makubwa.”

“Mwanzoni ilikuwa vigumu (wakati Messi alipoondoka). Ilikuwa mshtuko kwetu pia. Bado tuko hapa, lakini fikiria kwake; kubadilisha jiji, kubadilisha timu, kubadilisha mtindo.

“Usiposhinda huna furaha, namtakia kila la heri, ningependa Leo arudi lakini najua ni ngumu sana, ana mkataba na timu nyingine na ni ngumu kwa jinsi alivyoondoka.”

Mbali na kuchukizwa na taarifa za rafiki yake Mbappe kuhusishwa na safari ya kujiunga na Real Madrid msimu ujao, Messi mwenye umri wa miaka 34 bado hajawa kwenye kiwango chake kwenye ligi ya Ufaransa ‘Ligue 1’, akifunga mabao saba pekee katika mashindano yote akiwa na kikosi cha PSG chini ya Meneja Mauricio Pochettino.

Simba SC yakamilisha maandalizi ya vita
Kocha Pablo: Wachezaji wapo tayari kuivaa USGN