Hatimaye mashetani wekundu Man Utd, wamemtambulisha rasmi mlinda mlango kutoka nchini Argentina, Sergio Germán Romero baada ya kukamilisha taratibu za usajili wake ambao umekwenda sambamba na kusainiwa kwa mkataba wa miaka mitatu baina ya pande hizo mbili.

Mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 28, amesajiliwa na Man Utd baada ya kuwa huru kufuatia mkataba wake na klabu ya Sampdoria ya nchini Italia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu uliopita.

Meneja wa Man Utd, Louis Van Gaal amemtambulisha Romero mbele ya waandishi wa habari nchini Marekani ambapo kwa sasa kikosi chake kimeweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa ligi ya nchini Uingereza.

Van Gaal, amesema Romero ni chaguo sahihi katika mipango yake ya msimu ujao na ana matumaini atafanya kazi kwa dhati, ili kukamilisha mikakati ya kuirejeshea heshima klabu hiyo ambayo ilionekana kupoteza muelekeo kwa misimu miwili iliyopita tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi, aliwahi kufanya kazi na Romero wakati akiwa mkuu wa benchi la ufundi la klabu ya AZ Alkmaar baada ya kumsajili mwaka 2007 akitokea nchini kwao Argentina kwenye klabu ya Racing Club.

Hata hivyo, Van Gaal alimuacha Romero, baada ya kuondoka AZ Alkamaar na kutimkia nchini Ujerumani alipokwenda kukinoa kikosi cha FC Bayern Munich.

Romero alisalia klabuni hapo hadi mwaka 2011, kisha alijiunga na klabu ya Sampdoria ya nchini Italia.

Usajili wa Romero huko Old Trafford umelazimika kufanyika kufuatia mlinda mlango kutoka nchini Hispania, Victor Valdez kupishana kauli na Louis Van Gaal, hali iliyosababisha mkataba wake kuvunjwa.

Ramos aitikisa Real Madrid
Wojciech Szczesny Aliachia Goli La Arsenal