Raia wa falme ya Swaziland ambayo sasa inaitwa eSwatini, wataanza kutozwa fedha na Serikali ya nchi hiyo kwa kufunga ndoa na raia wa kigeni, endapo mswaada wa sheria ya fedha wa mwaka 2018 utapitishwa na kusainiwa kuwa sheria.
Kwa mujibu wa muswada huo, raia wa Swazi atakayetaka kufunga ndoa na raia wa kigeni atatakiwa kulipa ziada ya kiasi cha 30,000 lilangeni, fedha za Swazi, ili ndoa zao ziweze kuandikishwa na wizara ya mambo ya ndani.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mgwagwa Gamedze amekaririwa na gazeti la nchini humo akieleza kuwa sheria hiyo imelenga kuangazia ndoa kati ya raia wa nchi hiyo na raia wa kigeni.
Imeelezwa kuwa mswaada huo umepangwa kupitishwa haraka bungeni kabla ya Mfalme wa nchi hiyo kulivunja bunge mwezi ujao.
kwa sasa, raia wa nchi hiyo hulipwa kiasi cha lilangeni 100 kwa ajili ya kusajili ndoa zao na kupata vyeti.