Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ilifanya marekebisho ya sheria ya madini ya mwaka 2010 kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa  serikali katika sekta ya madini.

Ameyasema hayo jijini Dodoma katika uzinduzi wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ambapo amesema kuwa kwa mujibu wa marekebisho sambamba na kanuni zake za mwaka 2018 Bodi ya GST imeundwa ili kusimamia  utekelezaji wa majukumu ya GST.

Amesema kuwa uteuzi wa Rais kwa mwenyekiti na uteuzi wa waziri kwa wajumbe wa bodi umefanyika kwa mujibu wa sheria kwa kuzingatia vigezo vingi, ikiwemo uadilifu na uzalendo wao kwa nchi .

Aidha, mbali na hilo amesema kanuni za madini za mwaka 2018 zimeainisha wazi majukumu ya bodi hiyo ikiwemo kutathimini utendaji kazi wa GST, huku akisisitiza utekelezaji wa jukumu linalotokana na  marekebisho ya sheria ya  mwaka 2010.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Justin Ikingura amemhakikisha waziri kuwa yote aliyo yaeleza na kuyaagiza bodi itayazingatia na kufanyia kazi kwa ukamilifu pamoja na kusema kuwa wanatambua nia na lengo la  serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Rais Magufuli katika kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kukua na kutoa mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa.

 

Rais wa Comoro achaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo
Kanisa katoliki lamlipa billion 4 mwanaume aliyenyanyaswa kingono