Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel amesema katika mwaka 2023 Serikali imepanga kuajiri Wataalamu wa afya 12,000, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma kwa wananchi hasa maeneo yenye upungufu wa Watumishi na kupunguza changamoto ya ajira kwa Wataalamu wa afya nchini.
Dkt. Mollel amesema hayo hii leo Aprili 12, 2023 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maalumu, Minza Simon Mjika katika Mkutano wa 11 kikao cha tano.
Amesema, katika kuboresha huduma kwa wananchi katika kisiwa cha Ukerewe, Serikali imeipandisha hadhi iliyokuwa hospitali ya Wilaya hiyo na kuwa hospitali ya Mkoa, hali itayosaidia kuongezewa Wataalamu wa kutoa huduma, vifaa tiba na bajeti ya uendeshaji wa hospitali hiyo.
Aidha, Dkt. Mollel amesema, Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na OR TAMISEMI kuhakikisha mwananchi anapata huduma bora, kwa kuhakikisha maeneo yote yenye uhitaji hasa katika visiwa kunakuwa na zahanati katika kila kijiji na Wataalamu wa afya ili kupunguza kufuata huduma za afya kwa umbali mrefu.
Sambamba na hilo amesema, Serikali itaendelea kuwapanga watumishi katika Mikoa ya pembezoni mwa nchi kadri vibali vya ajira vitavyoendelea kutolewa kutokana na unyeti wa Mikoa hiyo kupakana na nchi nyingine hasa zenye milipuko ya magonjwa.