Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema Serikali imeendelea kuboresha mikakati ya kuokoa maisha ya watu kutokana na majanga mbalimbali, kwa kuanzisha Kitengo maalum kitakachoshughulika na kuokoa maisha ya watu kutokana na ajali.
Waziri Ummy, ameyasema hii leo Novemba 14, 2022 akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakati alipowatembelea majeruhi wa ajali iliyohusisha Basi la Arusha Express liligongana na Lori hapo jana Novemba 13, 2022 eneo la Mzakwe nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Amesema, “Katika Mipango yetu pale Wizarani, Kitengo cha Magonjwa yasiyoambukiza sasa hivi tutakiita Kitengo cha Magonjwa Yasiyoambukiza, Ajali na Afya ya Akili na ajali zinatokea lakini ni wajibu wetu ajali zinapotokea kuhakikisha tunatoa msaada wa haraka kwa majeruhi wa ajali, kwa hiyo hili ni eneo ambalo tutalipa kipaumbele.”
Ummy ameongeza kuwa, katika Wizara ya Afya ipo Idara ya Utayari na Udhibiti wa Majanga na Magonjwa ya Mlipuko na kuwataka wauguzi kutojikita kwenye kushughulikia magonjwa ya mlipuko pekee bali kuwa na mwitikio wa haraka kushughulikia majeruhi wa ajali.
Ameongeza kuwa, kupitia Idara hiyo, vilianzishwa vituo vya utayari na dharura kushughulikia majanga na ajali pembezoni na barabara kuu kutoka Dar Es Salaam hadi Mbeya hivyo kuwataka watalaam kuwa na mpango huo kwa barabara ya kuelekea Mkoa wa Dodoma.
Awali, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dkt. Ibenzi Ernest alisema Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 22 pamoja na watu 6 waliofariki ambapo kati ya majeruhi hao, mmoja alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Benjamin Mkapa na kwamba majeruhi 21 waliokuwa Hospitali hiyo, mmoja alifariki, tisa walipewa ruhusa na 11 wanandelea kupatiwa na matibabu.