Serikali kupitia Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji inaendelea kufanya maboresho sekta ya viwanda ili kuendana na kasi ya ujenzi wa uchumi wa viwanda hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Sekta ya Viwanda, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji Dkt. Adelhelm Meru wakati akifungua warsha ya siku moja ya tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo iliyofanyika mapema hii Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Meru amesema kuwa lengo la kufanya tathmini hiyo ni kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye viwanda vidogo na vya kati kwa kuwa kuna mabadiliko mengi yamefanyika tangu sera hiyo ianze kutumika mwaka 2003.

“Viwanda hivyo vinachangia asilimia 27 ya pato la taifa hivyo ni muhimu kupitia upya sera hii na kupata maoni ya wadau kwani hivi sasa kuna mabadiliko mengi ya teknolojia, sheria na taratibu za uwekezaji.” Amesema Dkt. Meru.

Aidha amesema kuwa Serikali itafungua dirisha dogo kwenye Benki ya Uwekezaji (TIB) kwa ajili ya kuwasaidia wawekezaji wa viwanda vidogo na vya kati kupata mitaji ya kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao.

Amesema kuwa Serikali ina mpango wa kuanzisha Benki ya Maendeleo ya Viwanda itakayowawezesha wazawa na wawekezaji wengine kupata mitaji yenye riba na masharti nafuu ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.

Hata hivyo, Dkt. Meru ametoa wito kwa Watanzania kujikita kwenye uwekezaji wa viwanda kwa kuwa ndio njia pekee ya kukuza uchumi kwa haraka na kuongeza ajira, teknolojia, biashara na mitaji.

Tathmini ya Sera ya Maendeleo ya Viwanda imekusudiwa kutoa mwelekeo wa namna bora ya kujikita kwenye uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wa viwanda vidogo na vya kati

Serengeti Boys Wachanjwa
Marc Wilmots Atangaza Ahadi Ivory Coast