Serikali kupitia Wizara ya afya imejipanga kukabiliana na ukosefu wa dawa muhimu katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mbele ya Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii wakati akiwasilisha randama ya bajeti ya Wizara mwaka wa fedha 2022/2023.
Waziri Ummy amekiri kuwa na uhaba wa dawa katika vituo vingi vya kutolea huduma za afya nchini huku sababu ikitajwa kuwa ni maoteo na kutozingatia mpango kazi wa manunuzi ya dawa pamoja na matumizi na usimamizi katika ngazi za vituo vya kutolea huduma za afya.
“Maoteo ya dawa yanatakiwa kuletwa Wizarani kutoka katika vituo vya kutolea huduma, tumeshaonesha magonjwa kumi yanayoongoza nchini hivyo inatakiwa kila kituo kijue ni magonjwa gani yanayoongoza kwa wananchi wa eneo hilo. Hivyo kituo kiweke mpango kazi wa manunuzi pamoja na matumizi sahihi ya dawa ili kuepusha kukosekana na kupelekea kero kwa wananchi”. Amesema Waziri Ummy.
Ameongeza kuwa ni jukumu la Mganga Mkuu wa Wilaya kupitia maoteo yanayoletwa kutoka katika vituo kama ni sahihi yaende ngazi ya Mkoa na kisha Wizarani Ili kusaidia Wizara kupanga bajeti ya dawa ambayo itakidhi mahitaji ya nchi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa afya Dkt. Godwin Mollel amesema mfumo wa ununuzi wa dawa katika bohari ya dawa (MSD) bado unaleta changamoto kwenye vituo vya kutolea huduma ambapo dawa zinapoagizwa hazifiki kama mahitaji yanavyotaka.
Dkt. Mollel amesema hali hii husababisha ukosefu wa dawa katika vituo na kuwafanya watoa huduma kuwaandikia wagonjwa fomu za kwenda kununua katika maduka binafsi.
Ili kutatua changamoto hiyo pamoja na nyingine Waziri Ummy ameiomba kamati ya kudumu ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii kupitisha bajeti ya Shilingi Trilioni 1.109 kwa ajili ya uendeshaji wa Wizara ya Afya ambapo wajumbe wa kamati wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti Aloyce Kamamba ilipitisha na kuwa bajeti rasmi ya mwaka 2022/2023.