Serikali imedhamiria kufikisha huduma za mawasiliano kwenye vijiji vyote nchini na maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara ili kuchochea ukuaji wa uchumi na utoaji wa huduma za kijamii kwa wananchi wote kwa wakati na uhakika kwa muda wote.

Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga wakati wa ziara iliyoandaliwa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia UCSAF ya kuwapeleka wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu kukagua maendeleo ya ujenzi wa minara ya simu za mkononi.

Amesema kuwa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wananchi na changamoto zilizopo kwa baadhi ya maeneo husika yatafanyiwa kazi ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata huduma za mawasiliano popote pale alipo.

Aidha, amesema kuwa hadi sasa UCSAF imejenga minara ya simu za mkononi kwenye maeneo saba yaliyopo Wilaya ya Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na kampuni za simu za mkononi.

Hata hivyo, Eng. Ulanga ameongeza kuwa Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutoa ruzuku kwa kampuni za simu za mkononi ili ziweze kufikisha mawasiliano kwenye vijiji vyote nchi nzima ambapo hadi hivi sasa UCSAF imetoa jumla ya dola za marekani milioni 41.5 ambazo ni sawa na shilingi bilioni 93.3 kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini kwenye kata 518 ambazo zitajengwa minara ya mawasiliano. Mpaka sasa jumla ya kata 391 kati ya kata 518 zimefikishiwa huduma ya mawasiliano katika kipindi cha miaka minne kuanzia mwezi Machi 2013 mpaka mwezi Agosti 2017 mwaka huu.

 

Video: Mbowe apinga kuondolewa kwa Lissu Kenya, anena mazito
Magazeti ya Tanzania leo Septemba 23, 2017