Serikali imesema kuwa katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ambapo taarifa za kila muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Igunga Dalaly Peter Kafumu, aliyetaka kupewa ufafanuzi juu ya Kwanini Serikali isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza utakasishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanywa nchi nyingi duniani.
“Msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali ili kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni 4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1” amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt Kijaji amesema kuwa Tanzania ina urari wa biashara ya nje ambao umetokana na sera huru za kigeni, ambazo zimechangia kuimarisha uchumi kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ulikua ni asilimia 7, ikiwa ni wastani wa juu sana ikilinganishwa na  nchi nyingine duniani.
 Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu na sio dola pekee huku akibainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha, hufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.

Kituo cha mabasi ya mikoani cha Temeke kuhamishiwa Mkuranga
Pombe za kienyeji sasa kukatiwa leseni