Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa taasisi binafsi na mashirika ya dini yaendelee kuangalia namna ya kupanga gharama za huduma wanazotoa zikiwemo za elimu na afya ili ziwiane na hali halisi ya vipato vya wananchi.
Ameyasema hayo wakati akizindua shule ya Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, ambapo amezindua shule hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli.
Amesema kuwa lengo la udhibiti huo ni kuimarisha viwango na ubora wa elimu inayotolewa, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali.
“Hivi sasa, Serikali kupitia vyombo mbalimbali inachukua hatua za makusudi za udhibiti ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma zenye viwango, ambapo baadhi ya wadau na wamiliki wanailalamikia Serikali kuwa inawakandamiza na kuwawekea masharti magumu,”amesema Majaliwa
Aidha, amesema kuwa utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA).
Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.