Serikali kwa kushirikiana na taasisi za sekta binafsi imeendelea kutoa elimu ya kilimo bora inayojumuisha matumizi sahihi ya mbolea za asili, viuatilifu vya asili, mbegu bora na hifadhi ya mazingira ili kuzalisha mazao kwa tija na kuwa na kilimo endelevu.
Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba wakati akijibu swali la Mbunge wa Chambani, Yussuf Salim Hussein aliyetaka kufahamu Serikali imeweka mikakati gani ya kutoa elimu ya mbolea ya asili kwa wakulima na hatua Serikali inayoichukua ili kuona kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuzalisha mazao yasiyotumia mbolea za viwandani.
Amesema kuwa katika kutekeleza mpango wa muda mrefu wa matumizi sahihi ya virutubisho vya udongo, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) inafanya utafiti wa afya ya udongo katika Kanda zote saba za kiikolojia za kilimo nchini.
Utafiti huo umelenga kubaini aina za virutubisho na tabia za udongo katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kutoa elimu kwa wakulima kuhusu kiasi, aina na matumizi sahihi ya mbolea za viwandani na asili. Utafiti huo umeanza kwa kuchukua sampuli za udongo katika Kanda za Nyanda za Juu Kusini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kaskazini na sehemu ya Kanda ya Mashariki (Mkoa wa Morogoro) na utaendelea katika maeneo mengine nchini na kukamilika Juni 2020.
Amesema kuwa kwa kutambua ongezeko la mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo zinazozalishwa kwa kutumia mbolea za asili na viuatilifu vya asili, Serikali imeboresha mtaala wa mafunzo katika vyuo vya kilimo ambapo mada za kilimo hai na hifadhi ya mazingira zimejumuishwa ili kuwawezesha maafisa ugani na wakulima kupata elimu hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Organic Agriculture Movemet (TOAM), Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), Ecology Agriculture chini ya SWISSAID, Zanzibar Organic Producers (ZANOP), Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO) na TANCERT inatoa elimu ya kilimo hai kwa wakulima na kutoa vyeti vya ubora wa mazao kwa ajili ya masoko maalum. baadhi ya mazao ambayo yanazalishwa katika mfumo wa kilimo hai hapa nchini ni pamoja na kakao, kahawa, pamba na viungo.
Hata hivyo, Bajeti za Wizara za Sekta ya Kilimo zinajumuisha bajeti za Wizara za sekta husika, Bodi za mazao na Taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara za Kisekta. Utekelezaji wa bajeti hizo huwawezesha wanaume na wanawake katika shughuli za kilimo. Wanawake wanachangia asilimia 90.4 ya nguvukazi ya wanawake inayotumika katika shughuli za kilimo na kuchangia wastani wa asilimia 70 ya mahitaji ya chakula nchini.
-
VIDEO: Askofu Gwajima ni MUATHIRIKA siyo MTUHUMIWA – Mambosasa
-
LIVE: MWILI WA DKT. MENGI UKIWASILI KILIMANJARO MUDA HUU
-
Habari picha: Hali inayoendendelea Dar kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha