Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kudumisha demokrasia nchini kwa kuyafanyia kazi mapendekezo na michango mbalimbali inayotolewa na vyama vya siasa, viongozi wa dini na asasi za kiraia kwa ustawi wa demokrasia.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo kwa niaba ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan wakati akifunga Mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 lililofanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo, umeandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania – TCD, kwa lengo la kujadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa maazimio ya Kongamano la kitaifa la Maridhiano, Haki na Amani na kuimarisha mapendekezo ya awali yaliyotolewa na wadau ili kuboresha mazingira ya kisiasa wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi mkuu 2025.
Vilevile, mkutano huo umehudhuriwa na Wawakilishi wa vyama vya siasa, viongozi kutoka Serikalini, Mabalozi na wadau wa demokrasia nchini ambapo Rais Dkt. Mwinyi pia amezindua mradi wa kuimarisha mazungumzo ya vyama vingi vya siasa na kukuza ushirikishi wa Wanawake na Vijana katika michakato ya kisiasa na chaguzi nchini.