Serikali imepanga kufunga kamera maalum za kurekodi matukio (CCTV Camera) katika barabara zote kuu nchini kwa lengo la kuwakamata wanaovunja sheria za barabarani.
Mpango huo umewekwa wazi na Naibu Waziri wa Kazi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa barabara ya ‘Old Mbalizi’ mkoani Mbeya.
Alisema kamera hizo zitakuwa zikifuatilia matukio ya magari yote ikiwa ni pamoja na mabasi ya abiria na magari binafsi, na kwamba madereva watakaokamatwa kwa kuvunja sheria hawatakwepa adhabu.
“Lengo la mradi huu ni kuhakikisha tunamaliza tatizo la ajali ambalo limekuwa likisababishwa na uzembe wa madereva kwa kiasi kikubwa. Ajali za mara kwa mara za barabarani zinagharimu nguvu kazi ya taifa letu,” alisema Naibu Waziri Kwandikwa.
Kwandikwa aliongeza kuwa wapo madereva ambao wameamua kukaidi na kutozingatia alama za barabarani. Hivyo, kwa CCTV Camera wanahakikishiwa kuwa watakamatwa na kuadhibiwa.
Aidha, alisema kuwa utekelezaji wa kuboresha barabara ya Mbalizi ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha ajali za barabarani zinapungua hasa katika eneo ambalo limekuwa likifahamika zaidi kwa kupata ajali.
“Tunafanya utambuzi wa maeneo ambayo yanapatikana ajali zaidi nchini na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha tunapunguza ajali za barabarani,” alisema.
Barabara hiyo yenye urefu wa Kilometa 6.5 ni maalum kwa ajili ya magari madogo. Ujenzi huo pia unaenda sambamba na ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa mizigo na magari ya abiria.