Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali inataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kupata tija.
Majaliwa amesema hayo wakati akikagua Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), iliyoanzishwa kwa lengo la kuimarisha masoko.
Amesema kupitia Wizara ya Kilimo, Serikali imedhamiria kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini ili kuwawezesha wakulima kujikwamua kiuchumi.
“Kupitia Wizara ya Kilimo tunataka kuimarisha masoko ya mazao yanayolimwa nchini. Wakati umefika kwa wakulima nchini kuona tija ya mazao wanayolima.”
Ametoa mfano wa zao la pamba ambalo wakulima walikuwa wanaingia mikataba na wanunuzi, mfumo ambao ulikuwa unawanyonya badala ya kuwanufaisha.
Kabla, Afisa Mtendaji Mkuu wa TMX, Godfrey Malekano alimuhakikishia Waziri Mkuu kwamba wamejipanga vyema kuanza minada ya mazao.
“Tutaanzia na zao la ufuta mwezi Mei 2018 na kuendelea na mazao mengine kwa kadiri ya misimu ya mazao hayo ilivyo.”
Amesema kufanikiwa kwa Soko la Bidhaa na Mfumo wa stakabadhi ghalani kunategemea sana msaada wa Serikali. “Soko la Bidhaa la Ethiopia linalotajwa sana kwa mafanikio, limefikia malengo yake kutokana na mkono wa Serikali.”
Malekano ameongeza kuwa kutokana na umadhubuti wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli wanamatumaini makubwa kwamba soko hilo litatimiza malengo yake.