Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, amesema Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa sekta za uwekezaji, biashara na utalii zinazidi kuimarika.
Kauli hiyo, imetolewa na Balozi wakati alipotembelea banda la Wizara katika maonesho ya 46 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam.
Waziri Mulamula, amewapongeza watumishi waliopo katika maonesho hayo na kusema Wizara inajivunia kuwa sehemu ya kutafuta wawekezaji na wafanyabiashara kuja nchini kama ambavyo kauli mbiu ya maonesho hayo inavyosema.
“Wizara kupitia Balozi zake Nje ya nchi inaendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali katika kuhakikisha kuwa tunapata wawekezaji wa kutosha kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, imejitahidi kuboresha mazingira ya biashara na uwekeza” amefafanua.
Hata hivyo, Waziri huyo amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa weledi na bidii ikiwemo kuzitangaza fursa za biashara, uwekezaji na vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini.
Awali, Balozi Mulamula alishiriki katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 46 ya Biashara ya Sabasaba yaliyofunguliwa na Katibu Mtendaji wa Sekretarieti ya Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), Wamkele Mene Juni 3, 2022 Mkoani Dar es Salaam.