Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali iliamua kufufua Shirika la Ndege la Tanzania ATCL kwa lengo la kupokea watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.
Rais Samia ameyasema hayo Julai 30, 2021 wakati wa hafla ya mapokezi ya Ndege aina ya Bombadier Dash 8-Q400 ikiwa ni ndege ya 9 kati ya Ndege 11 zilizonunuliwa toka serikali ya awamu ya tano hadi serikali ya awamu ya sita, amesema ili nchi iweze kunufaika na watalii wengi kuwa na ndege ni suala la muhimu.
Aidha Rais Samia amesema kuwa usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha mafanikio, kwa mujibu wa ripoti ya Banki ya Dunia 2018watu bilioni 4.52 walisafiri kwa kutumia ndege huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kufikia wasafiri Bilioni 20.7 mwaka 2040.
Amesema kuwa Tanzania imenunua ndege moja ya mizigo kwasababu ni moja ya nchi yenye uzalishaji mkubwa wa matunda , mboga mboga na maua, ambapo mwaka 2019 iliuza nje mazao yenye thamani ya dola za kimarekani miliioni 700,.
Hata hivyo serikali inataraji mwaka 2025 mazao yaingize dola za kimarekani billioni 2.