Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema serikali ipo katika majadiliano na mapitio ya sera ili kubadili sheria ya ndoa ambayo imekua ikileta changamoto katika kusimamia suala zima la ukatili wa watoto.

Amesema hayo akiwa katika mahojiano maalumu na Dar 24 akiongelea siku ya mwanamke duniani na uwepo wa wizara yake mpya kwa maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Mkanganyiko wa Sheria ya ndoa unaonekana na wadau wanaohusika wamefikisha malalamiko katika wizara hiyo na wapo katika mpango wa kuhakikisha sheria zote zinakwenda sambamba ili kuleta jamii yenye maridhiano na kupunguza ukatili.

“Malalamiko hayo tumeyapokea na yanaleta mijadala, hii sheria ya ndoa inasema mtoto aolewe na miaka 18, na nyingine miaka 14, hii inakinzana na ni moja ya changamoto katika juhudi hizi, hili ni eneo ambalo lipo mezani na tunalifanyia kazi pamoja na wadau ili kuona kwamba tunafanyaje ili zisigongane. Na baada ya hapo tutapeleka Bungeni ili waone wanapitishaje na sisi ni ‘machinery’ ya kuhakikisha kila wizara inakwenda sawa isiwe wizara hii inakwenda na A, mwingine B+ inakuwa mgongano, tafrani kwenya jamii, kwa hiyo siwezi kusema itakuwaje mbele ya safari ila tunalijadili,” amesema Dkt. Gwajima.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali ina mpango kazi wa Taifa wa kupinga ukatili kwa miaka mitano na kila mpango huo unaotekelezwa unafanyiwa tathmini ya yale yaliyofanyika kwa muhula na wakati mwingine masuala yaliyomo huendelea kwa kipindi kinachofuata.

Amesema katika mpango kazi unaeoeleka ukingoni kwa kipindi hiki umeangalia vipengele vyote vinavyoleta ukatili katika familia kama uchumi wa kaya, mila na desturi, elimu ya familia, ukeketaji, mazingira salama, malezi na mahusiano, utekelezaji wa usimamizi wa sheria, utoaji wa huduma kwa waathirika wa ukatili, mazingira salama shuleni, na uratibu na ufuatiliaji.

“Tumefanikiwa maeneo mengi katika hayo niliyoyataja, lakini suala la ukatili na huduma kwa waathirika wa ukatili, ilitakiwa kamati za kijamii ziundwe, na jukumu lake ndio kuangalia wapi pananukia ukatili, taarifa zimeletwa, na madawati ya jinsia yapo yameundwa, baadhi ya hospitali kubwa yana dawati la mkono kwa mkono na kesi zinashinda, tunashirikiana na wadau kwa namba 116 ambayo watu wanatoa taarifa kuhusu ukatili wa mtoto ambayo inasaidia kupunguza hizi kesi, kwa hiyo tumepokea taarifa nyingi sana katika eneo hili na tumeyashughulikia.

Aidha Dkt. Gwajima amesema katika maisha yake na wizara hii ya anayoisimamia suala la ukatili wa wanawake linamsumbua akili na analishughulikia kwa kila hali kuhakikisha linapungua na kuisha kwa haraka.

“Mimi ule ukatili anaopambana nao mwanamke, ukatili wa nguvu, Ukatili wa kiuchumi, mwanamke anaepambana kujiokoa yeye na watoto wake wakiwepoe wanaume, alafu wote hawa wakikua tena wanaanza kumkatili tena mwanamke aliehangaika nao. Mimi naanza kujiuliza huyu mwanamke aliyepitia madhila yote haya, mateso aliyoyapata mwanamke huyu mbona hakuwaacha watoto wake wa kiume? Amesema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima amesema kuwa kwa sasa majukwaa ya wanawake hayatoshi kukidhi na kujiondoa kwenye ukatili bali majukwa aya wanaume pia yanatakiwa kuongezeka ili wale ambao wanajua umuhimu wa kumtunza mwanamke wavunje ukimya na kuwapa elimu wengine ambao wanatenda ukatili huu.

“Hapa wanaume inabidi mjipange, tuzungumze, mnahitaji majukwaa ya wanaume pia ili wale wanaume wazuri wa fikra, kuna wanaumi wazuri sana, ili ule moto wa wanaume wazuri wa moyo, wa kutenda wa ‘break the silence’ wanazungumza ili hawa waovu wachache waone aibu isiwe dili tena, ili mwanaume akisimama nchini Tanzania aulizwe kwa vitendo vingapi vya ukatili ametenda, lazima tugeuze fikra zao, kwa sababu wengi wameshapandwa kwenye akili zao kuwa mwanamke ni duni,” ameongeza Dkt. Gwajima.

Dkt Gwajima ameongeza pia suala la ukatili lipo hata kwa wanawake kwa wanawake na chimbuko lake ni kwenye familia ambazo zimezoea kuona baba na mama wanafanyiana ukatili hivyo watoto bila kujali jinsia yao wanabebeshwa roho ya ukatili na kukua nayo hadi vizazi vyao vya baadae.

Waziri, Dkt. Dorothy Gwajima katika mahojiano studio za Dar24 Media

Simba SC yampa pole Hassan Dalali
Wanawake wahaswa kuhimiza wanaume kupima ukimwi