Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kisasa la wanafunzi katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalum katika shule ya msingi Mbugani iliyopo katika halmashauri ya Mji Geita mkoani humo.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wiliam Ole Nasha wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara hiyo mkoani Geita ambapo amesema kuwa fedha hizo zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuboresha elimu nchini.
Amesema kuwa serikali ya Awamu ya Tano inatambua umuhimu wa kuwajengea fursa na mazingira mazuri ya kusoma watoto wenye mahitaji maalum na ndio maana imeweka mkazo katika kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na vitabu ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo vyovyote kutokana na changamoto zao za kimaumbile.
“Kwa miaka mingi jamii nyingi zimekuwa zikiwatenga watoto wenye mahitaji maalum, lakini kwa sasa nashukuru tumeendelea kuwawezesha kupata haki yao ya Elimu kama walivyo watoto wengine na kwamba wanaweza kuwa na changamoto za kimaumbile lakini ubinadamu wao upo palepale,”amesema Waziri Ole Nasha.
Aidha, amewataka wanafunzi hao wenye mahitaji maalum kutokatishwa tamaa na changamoto walizonazo za kimaumbile kwani serikali imewawekea mazingira ya kuwawezesha kufika mbali zaidi katika Elimu na kuwataka kuendelea kutumia fursa hizo za kielimu ili kutengeneza maisha yao ya baadaye.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbugani, Edwicka Ndunguru amemweleza Naibu Waziri kuwa kituo hicho kilijengwa kwa lengo la kuwawezesha wanafunzi wenye mahitaji maalum kupata haki ya kielimu katika mazingira wezeshi na kuwapa fursa wengi zaidi wenye mahitaji maalum wanaoishi mbali na shule zinazotoa elimu maalum kupata elimu.
Amesema kuwa mafanikio ya kuwepo kwa vituo vya watoto wenye mahitaji maalum mbali na kuwawezesha kupata haki yao ya kielimu, pia imewasaidia kujifunza ujuzi mbalimbali, jamii imetambua nakuthamini umuhimu wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, kupata Elimu na wengine kufanikiwa kupata kazi katika maeneo mbalimbali.
Kituo hicho chenye vitengo vinne vyenye jumla ya wanafunzi 143 ambavyo ni vitengo vya ulemavu wa akili, Viziwi, ulemavu wa viungo na ulemavu wa macho, mbali ya kuhudumia wanafunzi hao wenye uwezo wa kufika shuleni lakini pia wanahudumia watoto 38 wenye ulemavu wa kiwango cha juu ambao hawawezi kufika shuleni hapo.