Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatarajia kuanza tathmini ya ujenzi wa ukuta katika fukwe za Bahari ya Hindi maeneo ya Nungwi Mkoa wa Kaskazini, Zanzibar.
Khamis amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua ni lini tathmni ya ujenzi wa ukuta katika maeneo yaliyoathiriwa na Bahari Nungwi na kusema fedha zimeshapatikana, andiko limewasilishwa kwa Wakala wa Majengo Tanzania – TBA, kwa ajili ya michoro kuainisha aina ya ukuta unaotakiwa kujengwa.
Naibu Waziri amefafanua kuwa kabla ya kujenga ukuta Serikali itafanya utafiti kujua ni aina gani ya ukuta unaofaa kujengwa katika eneo hilo ambao utasaidia kuzuia mawimbi yasifike kwenye makazi ya wananchi ili waendelee kufanya shughuli za kiuchumi.
Amesema, “Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika fukwe za Bahari ya Hindi. “Kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar imetenga shilingi milioni 650 kwa ajili ya tathmini ya awali ili kufanya usanifu wa miundombinu itakayosaidia kurudisha fukwe katika hali yake,” amesema Khams.
Aidha, amesema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, amewahimiza wananchi wa maeneo ya Nungwi kuongeza jitihada za kupanda mikoko ambao inasaidia kupunguza mawimbi ya bahari katika fukwe pamoja na kutochimba mchanga kiholela.
Pia, Naibu Waziri Khamis amewataka wananchi kuacha kutupa taka ovyo katika fukwe ili kulinda mazingira huku akiwapa rai kuhamasisha ulimaji na uvunaji wa mwani usioharibu fukwe na kuhimiza uongozi na wananchi wa Nungwi kuongeza jitihada za kutunza mazingira ya maeneo ya ufukwe kwa kudhibiti shughuli zisizo endelevu za kibinadamu kwa kuingeza jitihada za kuhifadhi mazingia na upandaji wa miti.