Eva Godwin – Dodoma.
Serikali Nchini, inatarajia kukamilisha sehemu ya mradi wa Nyumba 5,000 zinazojengwa katika Vijiji vya Msomera Wilayani Handeni (Tanga), Kitwai Wilayani Simanjiro (Manyara) na Saunyi Wilayani Kilindi (Tanga), hivi karibuni.
Akizungumza na Waandishi wa habari jijini Dodoma Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Mobhare Matinyi amesema Nyumba 503 zimeshajengwa na kuwezesha kaya 551 kuhamia zikiwa na watu 3,010 na mifugo 25,521 zote zikiwa kijijini Msomera.
“Ni vema kufahamu kuwa Kaya 27 zenye watu 120 na mifugo 769 tayari zilishahamia kwenye maeneo mengine nje ya hifadhi lakini si katika maeneo yaliyotengwa na serikali,” amesema.
“Wakazi wa kaya hizi walikwenda katika Wilaya za Karatu, Meatu, Monduli, Simanjiro, Handeni na mkoani Arusha, Hawa pia walisafirishwa na kulipwa fidia na malipo ya ziada,” amesema Matinyi
Aidha amesema kila kaya inayohamia katika maeneo yaliyotengwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapata: Malipo ya fidia Shilingi 10,000,000 za ziada kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Inasafirishiwa yenyewe pamoja na kila kitu chake, Inapewa nyumba ya vyumba vitatu kwenye eneo la ekari 2.5 pamoja na hati miliki, Inapewa shamba la ekari 5 pamoja na hati miliki, Inapewa eneo la kuchungia mifugo la jumla kwa wote pamoja na huduma za majosho na mabwawa ya kunyweshea mifugo”, amesema.
Hata hivyo amesema Serikali inajenga mnada wa mifugo wa kisasa,vituo vya kununulia maziwa,shule za msingi na sekondari, zahanati na vituo vya afya,barabara,na usalama kwa wananchi wote kwa kuweka vituo vya polisi.
Serikali inaendelea kusisitiza kuwa zoezi hilo ni la hiari na Wananchi waepukane na taarifa potofu kuwa kuna uvunjwaji wa haki za binadamu na uondoaji watu kwa nguvu.