Serikali imesema imeanza mchakato wa kukata rufaa kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Uingereza dhidi ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).
ATCL imeamriwa kulipa Dola Milioni 30.1 (takriban Tsh. Bilioni 69.23) kwa kampuni moja ya Liberia kama fidia baada ya kuvunjika kwa mkataba wa kukodisha ndege.
Kesi hiyo inahusu makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2013 na aliyekuwa Mkurugenzi wa ATCL, David Mattaka ya kukodisha ndege aina ya Airbus kutoka kampuni ya Willis Trading.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Uingereza, Christopher Butcher aliiamuru ATCL kulipa fedha hizo pamoja na riba inayoweza kufikia Dola Milioni 10 (Takriban Tsh. Bilioni 23) kwa kampuni hiyo ya Liberia, ambayo inajishughulisha na masuala ya kuuza na kukodisha ndege
Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi amesema mkataba wenyewe ulikuwa wa kifisadi wa kuitia nchi hasara na kusema hukumu hiyo imewashangaza kutokana na ukweli kuwa ndege yenyewe ilitumika kwa miezi saba tu.