Baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji uliokuwa unajengwa, Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa inatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kuanzia mwezi ujao.

Mradi huo unaojengwa kwa usimamizi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira, Manispaa ya Sumbawanga (SUWASA), kwa ufadhili wa nchi za Umoja wa Ulaya (EU) na Serikali ya Ujerumani kupitia benki yake ya Maendeleo (KfW), utagharimu sh. bilioni 31 utakapokamilika.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu  jana (Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati na akiweka jiwe la msingi la mradi wa maji safi na usafi wa mazingira katika Manispaa ya Sumbawanga na kuitaka kampuni ya kampuni ya Techno Fab Gammon Joint Venture ya India kumaliza ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.

Majaliwa alisema mradi huo ambao tayari umekamilika kwa asilimia 85 unatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu, hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanashirikiana na Manispaa katika kulinda miundombinu ya mradi huo mara utakapokamilika pamoja na kutunza vyanzo vya maji.

“Pamoja na Serikali kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji inayojengwa katika maeneo mbalimbali nchini,changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo imekuwa kubwa kutokana na baadhi ya visima vimeanza kukauka hali inayosababishwa na uharibifu wa mazingira,” – Majaliwa.

Alisema kumekuwa na uvamizi mkubwa katika maeneo ya vyanzo vya maji ambapo wananchi wanajishughulisha na shughuli za ulimaji, uchungaji wa mifugo, ujenzi wa nyumba za makazi na uchomaji misitu hivyo kusababisha uchafuzi wa mazingira na hatimaye vyanzo hivyo hukauka.

Hivyo, Waziri Mkuu amewaagiza wakuu wote wa wilaya na wenyeviti wa vijiji nchini kuyasimamia maeneo yenye vyanzo vya maji na kuwaondoa watu wotewalioyavamia kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwafikisha mahakamani.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Isack Kamwelwe aliyemuwakilisha Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge katika hafla hiyo alisema anaishukuru Serikali ya Ujerumani na Umoja wa nchi za Ulaya kwa kufadhili mradi huo.

“Wananchi wanatakiwa kuacha kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo kulima, kufuga ndani ya mita 60 kutoka katika mito, maziwa na vyanzo vingine vya maji ili kuepusha uharibifu wa mazingira ambao madhara yake ni makubwa kwa viumbe wote,”- Mhandisi Kamwelwe

Rais Magufuli ateua Kaimu Mkurugenzi NIDA
Mkuu wa Idara ya Ardhi apewa siku mbili kutatua matatizo ya ardhi, Rukwa