Serikali imeanza kufuatilia taarifa za uwepo wa abiria mmoja aliyerudi nyumbani nchini India akitokea Tanzania anayedaiwa kuwa na aina mpya ya kirusi cha UVIKO -19, Omicron.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Profesa Abel Makubi wakati akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu taarifa za abiria huyo.

Amesema bado haijajulikana kama abiria huyo alitokea Tanzania moja kwa moja au alipita Tanzania kuelekea India na haijajulikana alipita wapi kabla hajafika nchini India, hivyo Serikali kupitia vyombo vyake vya ndani inafanya uchunguzi wa kina.

Kwa mujibu wa Profesa Makubi, Serikali kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini India inafuatilia jambo hilo ili kubaini ukweli wake na baadaye kuchukua hatua stahiki.

Amewasihi Wananchi kutokuwa na hofu kutokana na taarifa hiyo ya kuwepo kwa abiria aliyerudi nchini India akitokea Tanzania mwenye aina mpya ya kirusi cha UVIKO -19, Omicron, bali waendelee kuwa watulivu na wafanye shughuli zao za kujiletea maendeleo huku wakichukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo.

Taarifa za uwepo wa abiria huyo zimechapishwa na kutangazwa na vyombo vya habari vya India na kuenea katika mitandao mbalimbali ya kijamii nchini.

Ukiwa kiongozi una maswali ya kujibu kwa Mungu- Rais Samia
Tahadhari ya corona kituo Cha mabasi mbezi Gwajima asikitishwa