Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeanza kupitia upya Sera ya Sekta ya Utalii Nchini ili kuhakikisha Sekta ya Utalii inakwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea duniani yakiwemo ya teknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki kwenye mkutano unaofanyika Jijini Arusha, amesema kuwa Sera inafanyiwa marekebisho kwa kuwa imepitwa na wakati kutokana na mabadiliko makubwa yaliyotokea katika Sekta hiyo.
Aidha, amesema kuwa kwa kutambua mchango wa Utalii kiuchumi, ni wazi kuwa Sera wezeshi ya Utalii yenye kutoa mwongozo wa utaratibu bora na sahihi wa usimamizi, uendelezaji na utendaji katika sekta hiyo unahitajika.
’’Tunataka kuibadilisha Sera hiyo ili iweze kujibu changamoto za aina ya Utalii wa sasa ambao kipindi cha nyuma haukuwepo, akitolea mfano Utalii mikutano pamoja na Utalii wa kiutamaduni ambao umekuwa ukikua kwa kasi hapa nchini,” amesema Dkt. Nzuki
Vilevile, Dkt. Nzuki amesema marekebisho ya Sera hiyo yanahitaji mchango mkubwa kutoka kwa wadau kwa kuwa inaendeshwa kwa kiasi kikubwa na sekta binafsi katika kutoa huduma na kufanya biashara za utalii hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Zahoro Kimwaga amesema uhuishwaji wa Sera hiyo utazingatia namna ambavyo wazawa wataweza kuwa wanufaika namba moja kwa kuwaandalia mazingira rafiki ya kuendesha biashara ya utalii tofauti na sasa ambapo makampuni mengi ya Utalii ni ya watu kutoka nje.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Richard Lugimbana amesema Sera iliyopo sio mbaya ila tatizo lililopo ni Serikali kushindwa kuitekeleza licha ya kuwa kuna baadhi ya vitu muhimu ambavyo havimo kwenye sera hiyo ikiwemo changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi.