Serikali imesema, ipo tayari kushirikiana na wadau kuboresha sekta ya maji na usafi wa mazingira nchini, ili kuwawezesha wananchi wa mijini na vijijini kuondokana na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ameyasema hayo wakati alipotembelea Chuo Kikuu cha Sayansi za Maisha cha Warsaw, nchini Poland katika siku yake ya kwanza ya ziara ya kikazi nchini humo.

Amesema, “Sekta ya maji na usafi wa mazingira ni miongoni mwa sekta za kipaumbele nchini, kwani zinagusa maisha ya wananchi wote wa mijini na vijijini kwani wanahitajika wawekezaji makini na wenye tija kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuiboresha.”

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax (kushoto), akiwa na Dkt. Hab Michal Zasada katika ziara yake ya kikazi nchini Poland.

Dkt. Tax ameongeza kuwa, miji mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma na Dar es Salaam inaendelea kukua kwa kasi hivyo upo umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye sekta hiyo ili kuwawezesha wananchi kupata maji safi na salama lakini pia kuendelea kutunza mazingira.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na Taasisi zinazosimamia sekta ya maji ikiwemo Wizara ya Maji ili kwa pamoja kuendelea kutafuta suluhu ya kudumu kwa changamoto zinazoikabili sekta hiyo kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje.

Dkt. Tax yupo nchini Poland kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 17 hadi 19 Oktoba, 2022, ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi baina ya nchi hizi mbili.

Kocha Juma Mgunda kuinusuru Simba SC Jumapili?
Polisi Tanzania yabadili upepo Ligi Kuu, yahamia Sokoine