Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Wizara ya Kilimo hapa nchini kufanikisha lengo lililowekwa na Wizara hiyo la kuacha kuuza Korosho ghafi nje ya nchi ifikapo mwaka 2026.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa wa Zao la Korosho unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam na kudai kuwa kuuza korosho isiyochakatwa (ghafi), kunasababisha kupunguza ajira za watanzania, kupunguza mapato ya fedha za kigeni pamoja na upatikanaji wa bidhaa zitokanazo na zao la korosho kama vile maziwa, mvinyo, juisi na mafuta.
Amesema, ni muhimu mkutano huo ukajadili na kubadilishana uzoefu wa namna ya kuimarisha huduma za ugani na utoaji pembejeo kwa wakati ili kuongeza uzalishaji wa zao la Korosho na kutoa wito kwa mkutano huo, kujadili namna bora ya kuwa na mkakati wa kufikia masoko ya zao la korosho kwa usawa.
Aidha, Dkt. Mpango amesema kumekuwa na ulaghai kati ya wanunuzi,wasafirishaji na madalali jambo linalothibitishwa na idadi ndogo ya wanunuzi kwenye minada ambao wana ufahamu wa kutosha kuhusu bei za soko huku wakulima wa korosho wakiwa na taarifa ndogo za soko na kwamba kutokana na hali hiyo, wakulima wa zao la korosho wamekabiliwa na bei isiyo ya haki.
Hata hivyo, amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya zao la korosho kutokana na taifa kuwa na ardhi ya kutosha ya kilimo na hali nzuri ya hewa na kwamba kipindi cha mavuno ya korosho nchini Tanzania (Septemba-Desemba) ni msimu wa kutokuwepo kwa wazalishaji wengine wakuu kama vile India, Vietnam na Afrika Magharibi hivyo kutoa fursa kubwa ya soko la zao hilo.