Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa yote ya Tanzania Bara, kukaa na Mabaraza ya Biashara na Wamiliki wa kumbi za Starehe katika mikoa yao ili kutafuta muafaka wa utekelezaji wa sheria, kanuni, mwongozo kuhusu udhibiti wa athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango.
Majaliwa ametoa maelekezo hayo wakati akizindua Kongamano la Kujengewa Uelewa kuhusu madhara yatokanayo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada ambapo pia amezielekeza Idara za Mipangomiji katika halmashauri za wilaya zote nchini zitenge maeneo ya ujenzi wa nyumba za ibada kama wanavyotenga maeneo ya taasisi nyingine.
Amesema, “kila mamlaka iliyotoa vibali au leseni ya shughuli au biashara, zifuatilie mwenendo wa matumizi ya leseni hizo. Nasisitiza kuwa kila mamlaka itimize wajibu wake kulingana na maelekezo yaliyimo katika Mwongozo wa Uthibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais.”
“Leo kuna kongamano la kitaifa linaloratibiwa na JMAT, NEMC wekeni mpango wa kufanya makongamano kama haya hadi katika ngazi ya mikoa ili jamii iwe na uelewa wa pamoja kuhusu athari za viwango vya sauti vinavyozidi. Aidha, toeni elimu kwa umma ili wajue viwango halisi vya sauti vinavyostahili wakati wa mchana na wakati wa usiku,” ameongeza Majaliwa.
Akizungumzia kuhusu wamiliki wa majengo, Waziri Mkuu amewataka wafanye tathmini ya athari ya mazingira kwa watu wanaotumia majengo hayo pamoja na wakazi wa jirani na majengo hayo kwa lengo la kubaini madhara kwa watumiaji wa majengo hayo na jamii inayozunguka.
Katika kongamano hilo liloandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania – JMAT, na kufanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi wa dini, wanaoshiriki katika kongamano hilo waendelee kuwa vielelezo na mabalozi wazuri wa kufikisha yale mambo mazuri yanayowasilishwa katika kongamano hilo.