Wakurugenzi wa Halmashauri na maafisa maendeleo ya jamii nchini wametakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ili viweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Serikali.

Katibu Mkuu ofisi ya Rais, tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga ametoa agizo hilo katika kongamano la asasi za kiraia (AZAKI) linalofikia tamati hii leo Novemba 8, 2019 Jijini Dodoma.

Amesema watu wenye ulemavu wamekuwa hawatumii fursa ya mikopo inayotolewa na Serikali hata katika Halmashauri zao kutokana na wengi wao kukosa na elimu ya ujasiriamali na ndio maana wengi wao wanaishia maisha ya utegemezi au kuomba mitaani.

“kwa kukosa Elimu ya ujasiriamali na hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha ikiwemo benki kutokana na hali yao ndiyo maana serikali iliamua kutenga asilimia 2 kati ya 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini ili kutoa mikopo kwa makundi maalum,” amefafanua Nyamhanga.

Amesema katika mwaka wa fedha 2018/19 Halmashauri nchini zilitenga sh. bilioni 54.08 kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu lakini mpaka kufikia Juni 30, 2019 kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa ni sh. bilioni 42.06 huku vikundi vya watu wenye ulemavu vikipata sh.Bilioni 3.87 pekee.

“Kwa mwaka wa fedha 2019/20 serikali imetenga kiasi cha fedha sh. bilioni 62.22 ambapo wanawake na vijana wametengewa sh. bilioni 24.9 na watu wenye ulemavu wametengewa sh. bilioni 12.4 hivyo utoaji wa elimu utasaidia kuwapa mwana na kujitokeza ili wapate mikopo,” amebainisha Katibu mkuu huyo wa TAMISEMI.

Awali Katibu Mkuu wa shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jonas Lubago ameungana na Nyamhanga kusema watu wengi wenye ulemavu hawana uelewa wa mikopo inayotolewa na Halmashauri nchini na ndiyo maana hawajitokezi kukopa.

Kufuatia hali hiyo ameomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwakopesha watu wenye ulemavu wakiwa mtu mmoja mmoja kutokana na wengi wao kushindwa kutumia fursa ya mikopo kwa kukosa vikundi vya kujiunga navyo.

Siri ya Arsene Wenger kwenda FC Bayern Munich yafichuka
LIVE KIBAHA: Maadhimisho Siku ya Malaria nchi za SADC