Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga amesema msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2020/2021 utazinduliwa tarehe 15 Juni 2020, ambapo serikali imejiweka kando kutopanga bei elekezi katika zao hilo pamoja na mazao mengine badala yake bei za mazao zitatokana na soko.
Ameyasema hayo leo Juni 7, wakati akizungumza kwenye mkutano maalumu wa wadau wa tasnia ya Pamba uliofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Benki kuu Jijini Mwanza.
Amesema kuwa kazi ya serikali ni kuhakikisha inasimamia uzalishaji bora wa mazao kadhalika kusimamia upatikanaji wa masoko ya mazao ili kuwa na bei nzuri yenye manufaa kwa wakulima.
Kutokana na usimamizi madhubuti wa serikali kupitia Wizara ya Kilimo, uzalishaji wa pamba umeongezeka kutoka tani 122,178 msimu wa ununuzi wa 2015/2016 hadi tani 348,910 msimu wa 2019/2020.
Amezitaja Hatua zilizochukuliwa na serikali kuwa ni pamoja na kuhamisha makao makuu ya Bodi ya Pamba kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza ili kuwa karibu na maeneo yanayolima pamba na kuwahudumia wakulima kwa karibu zaidi. Kutokana na hatua hiyo, ufanisi wa utendaji na huduma kwa wakulima umeongezeka.
Aidha ameeleza kuwa zao la pamba ni mhimili wa uchumi wa wananchi wengi katika mikoa 17 na Wilaya 56 zinazozalisha zao hilo.