Tanzania inakusudia kuanzisha programu jumuishi ya kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yenye lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote hususan katika ngazi ya msingi.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameyasema hayo jijini Geneva nchini Uswisi kwa njia ya mtandao katika kikao kilichoandaliwa na Shirika la Misaada na Maendeleo la Marekani – USAID, kwa kushirikiana na UNICEF.

Kikao hicho, kinahusu utekelezaji wa vipaumbele vya Azimio la Monrovia (2023), linalohusu Watoa Huduma wa Afya Ngazi ya Jamiii (Community Health Workers’ Roadmap).

Amesema, “Program hii inatarajia kuanza mwaka wa fedha 2023/24 na inalenga kuvifikia vijiji 12,318, mitaa 4,263 na vitongoji 64,384 nchi nzima.”

Kikao hicho, pia kimeshirikisha Mawaziri wa Afya, viongozi waandamizi wa Sekta ya Afya kutoka nchi 16 za Bara la Afrika, Asia na Mashirika ya Kimataifa kikijadili jinsi ya kuongeza rasilimali fedha, kuongeza ufanisi na tija katika utekelezaji wa miradi ya kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

Tunawatambua Wahandisi ukuzaji wa uchumi - Dkt. Mwinyi
Bil 4.5 zaanzisha huduma mpya ya upasuaji MOI